Mkuu wa ulinzi wa Ujerumani amesema kuwa wanachama wa muungano wa kijeshi wa Magharibi (NATO) wanapaswa kujiandaa kwa uwezekano wa kushambuliwa na Russia ndani ya kipindi cha miaka minne ijayo.
Jenerali Carsten Breuer aliambia BBC kuwa Russia inazalisha mamia ya mizinga (tanks) kila mwaka, na mingi kati ya hiyo inaweza kutumika kushambulia nchi wanachama wa NATO katika eneo la Baltic ifikapo mwaka 2029 au hata mapema zaidi.
Pia alisisitiza kuwa NATO – yaani Muungano wa Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini – bado umeungana kuhusu vita vya Ukraine, licha ya kuwepo kwa tofauti za maoni zilizotolewa hivi karibuni na Hungary pamoja na Slovakia.
Jenerali Breuer alikuwa akizungumza pembeni ya Mkutano wa Shangri-La Dialogue, mkutano wa masuala ya ulinzi unaofanyika nchini Singapore na kuandaliwa na taasisi ya utafiti ya International Institute of Strategic Studies.
Maoni yake yanakuja wiki chache kabla ya mkutano wa kilele wa mataifa ya NATO mjini The Hague, ambapo wanatarajiwa kujadili bajeti za ulinzi pamoja na masuala mengine.
Jenerali Breuer alisema kuwa NATO inakabiliwa na “tishio kubwa sana” kutoka kwa Russia, tishio ambalo hajawahi kuliona katika miaka yake 40 ya huduma.
Kwa sasa, alisema, Russia inajenga vikosi vyake kwa kiwango kikubwa sana, ikizalisha takriban mizinga mikubwa ya kivita 1,500 kila mwaka.
“Si kila tanki linaelekea [kwenye vita vya] Ukraine, bali pia linawekwa kwenye hifadhi na kwenye miundo mipya ya kijeshi ambayo kila wakati inakabili upande wa Magharibi,” alisema.
Russia pia ilizalisha makombora ya mizinga ya milimita 152 milioni 4 mwaka 2024, na si yote yalielekezwa Ukraine, aliongeza Jenerali Breuer.
Takwimu hizo zinatokana na wachambuzi wa Ujerumani na mataifa washirika.
“Kuna nia, na kuna mrundikano wa silaha,” kwa ajili ya uwezekano wa shambulio la baadaye dhidi ya nchi za NATO zilizoko Baltiki, alisema.
“Hivi ndivyo wachambuzi wanavyotathmini – mwaka 2029. Kwa hiyo tunapaswa kuwa tayari ifikapo 2029… Ukiniuliza sasa, je, kuna uhakika kwamba haitatokea kabla ya 2029? Ningesema hapana, hakuna uhakika. Kwa hiyo tunapaswa kuwa tayari kupigana hata usiku wa leo,” alisema.
Watu wengi kwa muda mrefu wameogopa shambulio dhidi ya taifa mwanachama wa NATO kwani linaweza kuchochea vita vikubwa kati ya Russia na Marekani, ambayo ni mwanachama muhimu wa NATO. Kulingana na Kifungu cha 5 cha mkataba wa NATO, shambulio lolote dhidi ya mwanachama mmoja linamaanisha kuwa wanachama wengine wote wanapaswa kuingilia kulinda.
Jenerali Breuer alitaja eneo la Suwalki Gap, linalopakana na Lithuania, Poland, Russia na Belarus, kama moja ya maeneo yaliyo hatarini zaidi.
“Eneo la mataifa ya Baltiki liko wazi sana kwa Warusi, sivyo? Na unapokuwa huko, unaliona hilo kwa kweli… katika mazungumzo tunayofanya huko,” alisema.
Alisema kuwa Waestonia walitoa mfano wa kuwa karibu na moto wa nyika, ambapo “wanahisi joto, wanaona miali ya moto na kunusa moshi”, huku nchini Ujerumani “pengine unaona moshi kidogo tu mbali na si zaidi ya hapo”.
Jenerali Breuer alisema hali hiyo inaonyesha mitazamo tofauti miongoni mwa mataifa ya Ulaya kuhusu tishio la shambulio kutoka kwa Russia.
Alisema mtazamo wa Russia kuhusu vita vya Ukraine ni tofauti na ule wa Magharibi, ambapo Moscow inaona vita hivyo kama sehemu ya mnyororo wa mgogoro mkubwa zaidi dhidi ya NATO, na hivyo “wanajaribu kutafuta mianya kwenye mistari yetu ya ulinzi na wanaijaribu”.
Alitaja mashambulizi ya karibuni dhidi ya nyaya za chini ya bahari katika Bahari ya Baltic, mashambulizi ya kimtandao dhidi ya usafiri wa umma barani Ulaya, na droni zisizojulikana zilizopatikana juu ya vituo vya umeme vya Ujerumani na miundombinu mingine.
Kwa hiyo, Jenerali Breuer alipendekeza kuwa wanachama wa NATO waanze kujenga upya majeshi yao. “Tunachopaswa kufanya sasa ni kuchukua hatua kwa dhati na kuwaambia kila mtu, hey, ongeza kasi… jitoe zaidi kwa sababu tunahitaji. Tunahitaji ili tuweze kujilinda, na hivyo pia kujenga uwezo wa kuzuia.”
Alipoulizwa na BBC kuhusu mshikamano wa NATO, kutokana na uhusiano wa karibu wa Hungary na Slovakia na Moscow, Jenerali Breuer alisisitiza kuwa muungano huo bado uko imara.
Alitaja uamuzi wa Finland na Sweden kujiunga na NATO mara tu baada ya vita vya Ukraine kuanza. “Sijawahi kuona umoja kama uliopo sasa” miongoni mwa mataifa na viongozi wa kijeshi, alisema.
“Wote wanaelewa tishio linaloelekea NATO kwa sasa, wote wanaelewa kwamba tunapaswa kuelekea kwenye uzuiaji wa mashambulizi, kuelekea katika ulinzi wa pamoja. Hili liko wazi kwa kila mtu. Dharura inaonekana.”
Kauli za Jenerali Breuer ni dalili nyingine ya mabadiliko makubwa ya mtazamo nchini Ujerumani kuhusu masuala ya ulinzi na Russia.
Kama mataifa mengi ya Magharibi, ikiwemo Uingereza, Ujerumani imepunguza uwekezaji wake katika jeshi kwa miaka mingi.
Lakini sasa kuna uelewa unaokua wa hitaji la kurekebisha hali hiyo, ambapo hata Chama cha Kijani (Green Party) kiliunga mkono kura ya hivi karibuni ya kuondoa vikwazo kwenye matumizi ya Ujerumani katika ulinzi.
Lakini wakati viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Magharibi wakisema wako tayari kwa mapambano, maswali bado yapo ikiwa huu ni mpango wa matumaini unaozidi uwezo wa utekelezaji.
Itachukua miaka kwa msingi wa viwanda vya kijeshi vya Ulaya kuweza kufikia kasi ya uzalishaji wa silaha ambayo Russia tayari inafanya.
Wakati huo huo, Marekani imekuwa ikipunguza, na si kuongeza, ahadi zake za kijeshi kwa Ulaya ili kuzingatia zaidi eneo la Indo-Pacific.
Comments
Post a Comment