Afisa mmoja mwandamizi wa Yemen amesema kwamba matumizi ya nguvu ndiyo njia pekee inayoweza kuzuia mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza, akisisitiza kuwa utawala wa Kizayuni unaelewa lugha ya nguvu pekee.
“Mashambulizi yasiyokoma dhidi ya Ukanda wa Gaza yanaweza kusitishwa tu kwa kuweka shinikizo la kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni, kwa kuwa wao hujibu tu kwa nguvu,” alisema Naibu Waziri wa Habari wa Yemen, Nasruddin Amer, siku ya Jumamosi.
Aliongeza: “Kwa neema ya Mwenyezi Mungu, Jeshi la Yemen litatumia uwezo wake wote kupanua wigo wa mapambano na kuongeza shinikizo kwenye ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Kwa njia hii, tunaweza kumaliza mateso na dhiki ya watu waliodhulumiwa wa Gaza.”
Jeshi la Yemen lilidai kuwajibika Alhamisi usiku kwa kufanya shambulio jipya la “kombora la kasi kubwa aina ya hypersonic” dhidi ya eneo la kati la ardhi zinazokaliwa na Israel, likisema kuwa lililenga Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion.
Msemaji wa jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, alisema katika taarifa iliyotangazwa na kituo cha televisheni cha al-Masirah kwamba taifa la Kiarabu litaendelea na mashambulizi yake “hadi uchokozi wa Israel dhidi ya Gaza utakaposita na mzingiro kuondolewa.”
“Tutaendelea kupiga marufuku safari za ndege za Israeli kwenda na kutoka Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion,” aliongeza Saree.
Kadri vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza vilivyozidi kupamba moto, Wayemen walitekeleza mzingiro wa kimkakati kwenye njia muhimu za baharini, ili kuzuia usafirishaji wa vifaa vya kijeshi kuelekea Israel na kuhimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kuhusu janga la kibinadamu linaloendelea huko Gaza.
Jeshi la Yemen limetangaza kuwa halitosita kushambulia hadi pale Israel itakapoacha mashambulizi yake ya ardhini na ya angani huko Gaza, ambako zaidi ya Wapalestina 54,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa.
Comments
Post a Comment