Shirikisho hilo pia limepiga marufuku mshindi wa dhahabu wa Olimpiki ya 2024 kushiriki mashindano yajayo hadi atakapopimwa.
Wanamasumbwi wa ridhaa wanaolenga kushiriki Olimpiki sasa watakabiliwa na vipimo vya kromosomu za jinsia, chini ya sheria mpya iliyowekwa na Shirikisho la Ngumi Duniani (World Boxing), ambalo ndilo shirika linalosimamia mchezo huo kimataifa.
Shirikisho hilo, ambalo litasimamia mchezo wa ngumi kwenye Olimpiki za Los Angeles mwaka 2028, limetaja wazi kwamba Imane Khelif kutoka Algeria – mwanamasumbwi ambaye uhalali wake wa kushindana kama mwanamke kwenye Olimpiki za Paris 2024 ulihojiwa – hataruhusiwa kushiriki hadi jinsia yake ya kijenetiki itakapothibitishwa.
Hatua hiyo mpya inalenga “kubaini uhalali wa wanamichezo wa kiume na wa kike wanaotaka kushiriki,” World Boxing ilieleza kupitia tovuti yake siku ya Ijumaa, ikifafanua kwamba kipimo hicho kinanuia kuhakikisha “usalama wa washiriki wote na… uwanja wa ushindani ulio sawa kwa wanaume na wanawake.”
Shirikisho hilo limesema vipimo hivyo vipo katika hatua za mwisho za maendeleo, na sheria mpya zitaanza kutumika kuanzia Julai 1.
Wale watakaobainika kuwa na “vinasaba vya kromosomu Y… au wana tofauti katika maendeleo ya kijinsia (DSD) ambapo kuna athari za homoni za kiume, wataruhusiwa kushindana katika kundi la wanaume,” World Boxing ilisema. Utaratibu huo utahusisha pia mchakato wa kukata rufaa na vipimo vya ziada endapo kutakuwa na pingamizi.
Uamuzi wa kuanzisha sheria hizo mpya ulifikiwa na bodi kuu ya utendaji ya Shirikisho la Ngumi Duniani mwezi Mei, kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo, likitaja kile walichokiita “hali ya dharura” na “hatari za kimwili zinazohusiana na ngumi za mtindo wa Olimpiki.” Mashirikisho ya kitaifa yatakuwa na jukumu la kufanya vipimo hivyo na yanaweza kuchukuliwa hatua ikiwa yatashindwa kufanya vipimo au yatatoa vyeti bandia.
Imane Khelif mwenye umri wa miaka 25 alipata umaarufu na utata katika Olimpiki za Paris alipomshinda mwanamasumbwi kutoka Italia, Angela Carini, ndani ya sekunde 46 pekee kwenye pambano la awali, jambo lililosababisha hasira kubwa mitandaoni. Baadaye alishinda medali ya dhahabu katika kitengo cha wanawake.
Kwa mujibu wa mamlaka za Algeria, Khelif si mtu aliyejibadilisha jinsia (transgender), bali ana hali ya kiafya inayosababisha kiwango kikubwa cha homoni ya testosterone na uwepo wa kromosomu za XY. Alifeli kwenye kipimo cha jinsia na akatolewa kwenye mashindano na Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBA) – ambalo awali ndilo lililosimamia ngumi za Olimpiki. Hata hivyo, baadaye aliruhusiwa kushiriki kwenye Olimpiki za Paris.
Khelif mwenyewe alikanusha tuhuma zote na hata kufungua kesi mahakamani akilalamikia kile alichokiita “matendo ya unyanyasaji mkali wa kimtandao” kutoka kwa watu mashuhuri kadhaa, wakiwemo Elon Musk na mwandishi wa riwaya za Harry Potter, J.K. Rowling.
Comments
Post a Comment