Mwanamke mmoja wa Afrika Kusini ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumuuza binti yake mdogo.

Mwanamke mmoja wa Afrika Kusini amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumuuza binti yake wa miaka 6, katika kesi iliyotikisa taifa hilo.

Kelly Smith, ambaye jina lake kamili ni Racquel Chantel Smith, alihukumiwa pamoja na mpenzi wake, Jacquen Appollis, na rafiki yao, Steveno van Rhyn. Wote watatu walipokea hukumu ya kifungo cha maisha kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu, na adhabu ya ziada ya miaka 10 kila mmoja kwa kosa la utekaji nyara. Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Nathan Erasmus katika mji wa Saldanha Bay, ulioko pwani ya magharibi ya Afrika Kusini, ambako kesi hiyo ilihamishiwa kwenye uwanja wa michezo wa jamii ili kuruhusu wakazi kuhudhuria.

Joshlin, binti wa Smith, alitoweka mwezi Februari 2024, jambo lililoanzisha msako wa kitaifa. Hapo awali, Smith alionekana kama mwathirika, na wanajamii wengi walijitokeza kusaidia polisi kumtafuta msichana huyo katika kitongoji chao maskini kilicho karibu na Saldanha Bay. Picha ya Joshlin akiwa anatabasamu huku nywele zake zikiwa zimefungwa pigtail ilisambaa kote Afrika Kusini wakati wa msako huo.

Hata hivyo, kesi hiyo ilichukua mwelekeo wa kutisha Smith alipokamatwa. Wakati wa kesi, shahidi mmoja alieleza kuwa Smith alikiri kumuuza binti yake kwa pamoja na wanaume hao wawili kwa takribani dola 1,000 kwa mganga wa kienyeji aliyedaiwa kuhitaji mtoto huyo kwa ajili ya viungo vya mwili wake.

Uamuzi wa jaji haukufafanua ni nani hasa aliyenunua mtoto huyo wala kilichomtokea, lakini ulithibitisha kuwa aliuza kwa madhumuni ya utumwa au vitendo vinavyofanana na utumwa. Hadi leo hii, Joshlin bado hajapatikana. 

Comments