Bilionea huyo wa teknolojia anapanga kuwekeza zaidi ya dola bilioni 200 kufikia mwaka 2045, kwa miradi inayolenga kilimo na upanuzi wa matumizi ya teknolojia ya AI katika sekta ya afya barani Afrika.
Bilionea wa Marekani, Bill Gates, ametangaza mipango ya kutumia sehemu kubwa ya utajiri wake katika kipindi cha miaka ishirini ijayo ili kuimarisha mifumo ya afya na elimu barani Afrika, ambako baadhi ya miradi ya awali ya taasisi yake imewahi kukosolewa.
Mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft alitoa ahadi hiyo katika hotuba yake kwenye hafla iliyoandaliwa katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, jijini Addis Ababa, Ethiopia, siku ya Jumatatu, akisema kuwa lengo lake ni kusaidia kila nchi barani humo kuingia kwenye “njia ya mafanikio.”
“Nimeweka ahadi hivi karibuni kwamba utajiri wangu wote utatolewa ndani ya kipindi cha miaka 20 ijayo. Sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika kuwasaidia kushughulikia changamoto hapa Afrika,” alisema, akibainisha kuwa utajiri wake umefikia “kiwango cha juu sana.”
Taasisi ya Gates ilitangaza mwezi uliopita kuwa itafanya uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 200 kufikia mwaka 2045, mwaka ambao inapanga kumaliza shughuli zake. Fedha hizo zitazingatia kupanua upatikanaji wa chanjo, kuboresha afya ya mama na mtoto, kuimarisha elimu – hasa kwa wasichana – na kujenga miundombinu ya kidijitali kusaidia mifumo ya afya ya umma.
Ahadi hiyo inakuja wakati ambapo misaada ya kimataifa kwa Afrika inapungua, jambo lililoangaziwa na uamuzi wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kupunguza zaidi ya asilimia 90 ya mikataba ya misaada ya kigeni ya USAID. Hatua hiyo ya serikali ya Marekani imesababisha kusitishwa kwa miradi mingi ya afya na maendeleo duniani kote.
Taasisi ya Gates, ambayo ni miongoni mwa wachangiaji wakubwa wasio wa kiserikali kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), imekuwa ikihusika katika juhudi za kupambana na magonjwa kama vile malaria, UKIMWI, na polio, sambamba na kufadhili miradi ya utafiti na usambazaji wa chanjo.
Hata hivyo, shirika hilo lisilo la kiserikali limejikuta likikabiliwa na utata kuhusu baadhi ya miradi yake. Makundi ya watetezi wa haki yamelituhumu kwa kuendeleza kilimo cha mazao yaliyobadilishwa vinasaba (GMO) na mifumo ya kilimo cha kibiashara ambayo hunufaisha makampuni makubwa huku wakulima wadogo wakiachwa nyuma.
Wakosoaji pia wameelezea wasiwasi kuhusu ushawishi mkubwa wa taasisi hiyo katika sekta ya afya duniani – ikiwa ni pamoja na madai ya kuwa na ushawishi ndani ya Shirika la Afya Duniani (WHO) – wakitaja ukosefu wa uwajibikaji wa kutosha katika kuzuia na kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na miradi yake.
Jumatatu, Gates alisema lengo lake ni kusaidia Afrika kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya kuuza nje, kwa kuwapatia wakulima mbegu bora, vifaa, na taarifa sahihi. Bilionea huyo wa teknolojia aliwahimiza wabunifu wa Afrika kufikiria namna ya kujenga Teknolojia ya Akili Bandia (AI) kwa ajili ya kuboresha huduma za afya barani humo, akisema kuwa taasisi yake inalenga kusaidia vipaji bora vya AI ili kuhakikisha teknolojia hiyo inanufaisha kila mtu – siyo mataifa tajiri pekee.
Comments
Post a Comment