London yasaini makubaliano ya kurejesha mamlaka ya Chagos kwa Mauritius, huku ikibakiza mkataba wa miaka 99 wa Diego Garcia
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, asaini makubaliano ya kurejesha visiwa vya Chagos kwa Mauritius
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alisaini makubaliano siku ya Alhamisi ya kuhamisha rasmi mamlaka ya Visiwa vya Chagos kwa Mauritius. Hata hivyo, makubaliano hayo yanaruhusu Marekani na Uingereza kuendelea kudhibiti kwa pamoja kambi ya kijeshi kwenye kisiwa cha Diego Garcia kwa kipindi cha awali cha miaka 99.
Visiwa vya Chagos, ambavyo ni zaidi ya visiwa 60 vilivyoko katika Bahari ya Hindi, takriban maili 310 kusini mwa Visiwa vya Maldives, vilitenganishwa na Mauritius na Uingereza mnamo mwaka 1965, kabla Mauritius haijapata uhuru wake mwaka 1968. Tangu wakati huo, Mauritius imekuwa ikidai kurejeshewa eneo hilo. Mwaka 1966, kisiwa kikubwa zaidi, Diego Garcia, kilikodishwa kwa Marekani, na takriban wakaazi 2,000 walifukuzwa.
Keir Starmer alisisitiza umuhimu wa kimkakati wa Diego Garcia, akisema kuwa:
“Mahali ilipo kambi hii ni muhimu sana kwa Uingereza — iwe ni kwa ajili ya kurusha ndege za kijeshi kupambana na magaidi huko Iraq na Afghanistan, au kwa kutambua mapema vitisho katika Bahari Nyekundu na eneo la Indo-Pasifiki.”
Aliongeza pia kuwa makubaliano hayo yanahakikisha ulinzi madhubuti dhidi ya ‘ushawishi mbaya’ (malign influence).
Akizungumza kutoka makao makuu ya kijeshi ya Northwood nchini Uingereza, Waziri Mkuu Keir Starmer alisema kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, pia anaunga mkono makubaliano hayo, akitambua umuhimu wa kimkakati wa kambi hiyo ya kijeshi.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Mauritius, Navin Ramgoolam, aliyaelezea makubaliano hayo kama hatua ya kihistoria, akisema:
“Kupitia makubaliano haya, tunakamilisha mchakato wa ukombozi dhidi ya ukoloni.”
Hata hivyo, wakosoaji wa makubaliano hayo, wakiwemo msemaji wa masuala ya mambo ya nje wa Chama cha Conservative, Priti Patel, walieleza kuwa makubaliano haya ni ya gharama kubwa na yanahatarisha ushawishi wa kimkakati wa Uingereza katika eneo hilo, hususan dhidi ya China.
Patel aliita makubaliano hayo "Makubaliano ya Kujisalimisha kwa Labour kuhusu Chagos," akisema kwamba ni:
"Mabaya kwa ulinzi wa Uingereza, kwa walipa kodi wa nchi, na kwa raia wa Chagossian wa Uingereza."
Kwa mujibu wa shirika la habari Reuters, thamani ya jumla ya makubaliano hayo inakadiriwa kufikia dola bilioni 3.9 (sawa na pauni bilioni 3) kwa kipindi cha miaka 99.
Makubaliano hayo yanajumuisha eneo la usalama la maili 24 kuzunguka kisiwa cha Diego Garcia, ambapo hakutakuwa na ujenzi wowote bila idhini ya Uingereza.
Pia kuna chaguo la kuongeza muda wa mkataba kwa miaka 40 zaidi, iwapo pande zote mbili zitakubaliana.
Comments
Post a Comment