Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai kuwa washauri wa Rais wa zamani Joe Biden walifanya usaliti kwa kumtumia vibaya mtangulizi wake ambaye, kwa mujibu wa Trump, alikuwa na "udhaifu wa kiakili."
Rais wa Marekani, Donald Trump, amewatuhumu wasaidizi waandamizi wa mtangulizi wake, Joe Biden, kwa kutenda "usaliti wa juu kabisa", akidai walitumia kupungua kwa uwezo wa kiakili wa Biden kusukuma sera ambazo hakuziunga mkono binafsi.
Kupitia chapisho katika jukwaa lake la Truth Social siku ya Jumanne, Trump alidai kuwa Biden hakuwahi kuunga mkono sera za mipaka wazi, na kwamba ongezeko la wahamiaji haramu lilipangwa na washauri wake waliodhibiti kifaa cha “autopen” – mashine inayoweza kusaini kwa niaba ya mtu – ili kusaini maagizo bila ridhaa ya rais mwenyewe.
“Joe Biden ambaye kila mtu alimjua asingekubali wauzaji wa dawa za kulevya, wanachama wa magenge, na watu wenye matatizo ya akili kuingia nchini mwetu bila kukaguliwa kabisa,” Trump alisema. “Kila mtu anaweza tu kuangalia rekodi yake.”
Aliongeza kuwa wimbi hilo la wahamiaji haramu limeigharimu Marekani “mamia ya mabilioni ya dola.”
“Haikuwa wazo lake kufungua mpaka… Ilikuwa ni watu waliokuwa wanajua kuwa hana uwezo wa kiakili, na walichukua udhibiti wa autopen,” Trump alidai. “Huu ni USALITI wa kiwango cha juu!... Lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahaini hawa waliotaka kuiangamiza nchi yetu, lakini walishindwa kwa sababu mimi nilikuwepo.”
Rais wa Marekani Donald Trump ameendeleza tuhuma zake dhidi ya utawala uliopita, wakati huu akichochewa na taarifa za hivi karibuni kuhusu afya ya Joe Biden. Biden ametangazwa kuwa na saratan ya tezi dume ya aina kali, yenye Gleason score ya 9 na imeshasambaa hadi kwenye mifupa. Ingawa Trump alitoa matamshi ya kumtakia Biden afya njema hadharani, pia alihoji muda na uwazi wa kutolewa kwa taarifa hiyo, akidokeza kuwa umma haukujulishwa mapema vya kutosha.
“Nimeshangazwa kwamba… umma haukuarifiwa mapema, kwa sababu kufika hatua ya tisa (stage nine), hiyo ni safari ya muda mrefu,” Trump aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu, akihoji namna madaktari wa Ikulu ya White House na Hospitali ya Jeshi ya Walter Reed walivyoshindwa kugundua hali ambayo huchukua miaka kujitokeza.
Trump pia aliendeleza hoja yake kuhusu matumizi ya kifaa cha autopen, akisema:
“Autopen sasa limekuwa jambo kubwa sana. Unajua, autopen linaonekana kuwa jambo kubwa kwa sababu huenda ndiyo iliyokuwa ‘rais’ – yaani yule aliyeendesha autopen.”
Aliongeza kuwa kuna uwezekano madaktari haohao walikosa pia dalili za kupungua kwa uwezo wa kiakili wa Biden:
“Kwa maneno mengine, kuna mambo yanaendelea ambayo umma haukufahamishwa. Na nafikiri kuna mtu atakayelazimika kuzungumza na daktari wake.”
Kauli hizi zimeongeza mvutano wa kisiasa unaoendelea kuelekea uchaguzi wa urais, huku Trump akiweka mashaka juu ya afya, uhalali wa uongozi, na uaminifu wa utawala wa Biden.
Kifaa cha autopen – kinachotumika kusaini nyaraka kwa niaba ya rais – kimekuwa kitovu cha mashambulizi mapana ya Rais Donald Trump dhidi ya utawala wa Joe Biden. Mapema mwaka huu, Trump alitangaza kwamba baadhi ya msamaha wa dakika za mwisho uliotolewa na Biden hauna uhalali, akidai kuwa ulitiwa saini bila rais mwenyewe kujua.
Wataalamu wa sheria wanasema kuwa matumizi ya autopen na marais wa Marekani yana historia ya muda mrefu na ni halali kisheria iwapo rais ametoa idhini. Hata hivyo, Trump anasisitiza kuwa katika utawala wa Biden, kifaa hicho kinaweza kuwa kilitumika vibaya na wasaidizi waliokuwa wakifanya maamuzi yao binafsi bila idhini ya rais.
Hali hiyo imeibua wasiwasi mkubwa wa kisiasa, na sasa Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya Bunge la Wawakilishi, James Comer, ameanzisha uchunguzi rasmi kuchunguza iwapo wasaidizi wa juu wa Biden walihusika katika kuficha hali ya kushuka kwa uwezo wa kiakili wa rais huyo.
Uchunguzi huo unaweza kuwa na athari kubwa kisiasa na kisheria, hasa wakati Marekani ikielekea kwenye uchaguzi wa rais, huku afya na uwezo wa Biden kuwa suala linalozidi kuvuta hisia za umma na vyombo vya habari.
Comments
Post a Comment