Trump asema ushuru wa 80% dhidi ya China "unaonekana sahihi" kabla ya mazungumzo ya kibiashara

Kabla ya mazungumzo muhimu ya kibiashara kati ya China na Marekani yaliyopangwa kufanyika mwisho wa wiki hii, Rais Donald Trump amependekeza ushuru wa asilimia 80 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka China kama mbadala wa kiwango cha sasa cha asilimia 145, akisisitiza kuwa kiwango hicho kipya “kinaonekana sahihi.”

“Ushuru wa 80% kwa China unaonekana sahihi!” aliandika Rais Donald Trump kwenye jukwaa lake la mitandao ya kijamii, Truth Social, siku ya Ijumaa.

“Mikataba mingi ya biashara iko jikoni, yote ni mizuri (MIZURI SANA!)!” aliongeza.

Hata hivyo, alisema kuwa jukumu la kufanikisha jambo hilo liko mikononi mwa Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent.

Ujumbe wa Trump unakuja wakati ambapo Bessent, akiandamana na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, anatarajiwa kukutana na maofisa wa China kujadili makubaliano ya kibiashara.

Pande hizo mbili zimepanga kukutana mwishoni mwa wiki hii huko Uswisi kwa ajili ya kutafuta njia za kumaliza vita vya kibiashara vinavyoendelea kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeeleza wasiwasi wake kuhusu “habari za kupotosha” zinazosambazwa na Trump kuhusu hali halisi ya mikataba ya kibiashara.

Beijing imeonya kuwa haitavumilia vitisho wala mashinikizo kutoka kwa utawala wa Trump, ikisema haitakubali “kulazimishwa au kutishwa.”

Tangu alipochukua madaraka mwezi Januari, Trump ameongeza ushuru kwa bidhaa kutoka China hadi asilimia 145, akiongeza juu ya ushuru alioweka wakati wa muhula wake wa kwanza na yale yaliyowekwa na utawala wa Biden.

Kwa kujibu, China imeweka vikwazo vya usafirishaji wa malighafi adimu za viwandani (rare earth elements) zinazohitajika kwa utengenezaji wa silaha na vifaa vya kielektroniki vya Marekani. Pia, imepandisha ushuru kwa bidhaa za Marekani hadi asilimia 125, na kuongeza kodi ya ziada kwa bidhaa kama maharage ya soya na gesi asilia iliyoloweshwa (LNG).

Mkakati wa ushuru wa Trump unachukuliwa na wengi kuwa hatari kwa uchumi wa Marekani, ukizua hofu ya kuongezeka kwa gharama za bidhaa kwa watumiaji na biashara, na huenda ukapunguza mahitaji, jambo ambalo linaweza kuathiri vibaya soko la ajira.

Trump pia anakabiliwa na kuporomoka kwa umaarufu, huku Wamarekani wakijiandaa kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali kama mavazi, vifaa vya kielektroniki na hata vinyago, kutokana na ongezeko la ushuru kwa bidhaa kutoka China.

 

Comments