Taasisi hiyo ya Ivy League imepewa saa 72 kutii matakwa ya Ikulu ya Marekani.
Ikulu ya Marekani imefuta kibali cha Chuo Kikuu cha Harvard cha kuandikisha wanafunzi wa kimataifa, hatua inayozidisha mvutano unaoendelea kati ya taasisi hiyo ya Ivy League na serikali kuhusu madai ya kupuuza chuki dhidi ya Wayahudi (antisemitism) na kukataa kuvunja programu za utofauti, usawa, na ujumuishaji (DEI).
Tangu kurejea madarakani, Rais wa Marekani Donald Trump ameyataka vyuo vikuu kusitisha maandamano ya kupinga Israel, ambayo ameyataja kuwa ya chuki dhidi ya Wayahudi, na pia kuvunja programu za DEI ambazo anadai zinachochea "mgawanyiko na msimamo mkali."
Katika tamko la Alhamisi lililotolewa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Kristi Noem, Harvard ilipewa saa 72 kutekeleza masharti ya serikali ya shirikisho ili kibali chake cha kushiriki katika Mpango wa Wanafunzi na Wanaobadilishana (SEVP) kiweze kurejeshwa. Miongoni mwa masharti hayo ni kuwasilisha rekodi zote za kinidhamu za wanafunzi wa kigeni kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, pamoja na ushahidi wowote wa kielektroniki, video au sauti unaoonyesha ushiriki wao katika matendo ya “kukiuka sheria, kuwa hatarishi, au ya vurugu” chuoni.
“Harvard haiwezi tena kuandikisha wanafunzi wa kigeni, na waliopo sasa lazima wahamie vyuo vingine au wakabiliane na kupoteza hadhi yao ya kisheria nchini,” Noem aliandika katika barua kwa Rais wa Harvard, Alan Garber, tarehe 22 Mei. “Hii iwe onyo kwa vyuo na taasisi zote za elimu kote nchini.”
"Utawala huu unakishikilia Chuo Kikuu cha Harvard kuwajibika kwa kuchochea vurugu, chuki dhidi ya Wayahudi, na kushirikiana na Chama cha Kikomunisti cha China katika mazingira ya chuo chake," alisema.
Kufutwa kwa cheti cha SEVP cha Harvard kunaweza kuathiri takriban wanafunzi 6,800 wa kimataifa walioko katika chuo hicho kilicho Cambridge, Massachusetts, ambao wanajumuisha takriban asilimia 27 ya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa masomo 2024–25.
“Ni heshima, si haki, kwa vyuo kuandikisha wanafunzi wa kigeni na kufaidika na malipo yao ya ada ya juu ambayo huchangia kuongeza hazina zao za mabilioni ya dola,” alisema Noem.
Harvard imekata rufaa hatua hiyo kama isiyo halali na ya kulipiza kisasi kisiasa, ikisisitiza kuwa hatua za serikali zinahatarisha kazi ya kitaaluma ya chuo na hadhi yake duniani.
“Tumejitolea kikamilifu kuhakikisha Harvard inaendelea kuwa na uwezo wa kuwahudumia wanafunzi na wasomi wa kimataifa, wanaotoka zaidi ya nchi 140 na kuleta mchango mkubwa kwa Chuo hiki – na taifa hili,” alisema msemaji wa Harvard, Jason Newton, katika taarifa yake.
Mvutano huu unaashiria ongezeko kubwa la shinikizo kutoka kwa utawala wa Trump dhidi ya vyuo vikuu vya ngazi ya juu, huku kukiwa na mwitikio mkali wa kisiasa kuhusu jinsi vyuo hivyo vilivyoshughulikia maandamano ya wanafunzi wanaounga mkono Palestina.
Baada ya Harvard kukataa masharti ya serikali ya shirikisho na kuahidi kushughulikia matatizo yake ya ndani kwa njia yake mwenyewe, serikali ilizuwia ufadhili wa dola bilioni 2.2 kutoka kwa serikali kwa chuo hicho, sehemu ya uhakiki mpana wa karibu dola bilioni 9 za misaada ya umma iliyotolewa kwa Harvard na taasisi zake za utafiti zinazohusiana.
Comments
Post a Comment