Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza Jumapili kuwa limekamilisha makubaliano ya ushirikiano na Tume ya Ulaya kwa ajili ya michuano kadhaa ya soka ijayo barani Afrika.
Umoja wa Ulaya utadhamini Mashindano ya Soka ya Shule za Afrika, pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika la mwaka 2025 na 2027, na pia mashindano ya wanawake ya mwaka huu.
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake litafanyika mwezi Julai 2025 nchini Morocco, likifuatiwa na toleo la wanaume mwezi Desemba. Mashindano yote mawili yana mdhamini mkuu, kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa, TotalEnergies.
Makubaliano hayo yalisainiwa na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na Ushirikiano wa Kimataifa, Jozef Síkela, pamoja na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, jijini Cairo, Misri.
Katika taarifa yake, Motsepe alisema:
"Ushirikiano wetu unaakisi dhamira ya pamoja kati ya CAF na Tume ya Ulaya katika kukuza na kuendeleza Soka la Shule na Vijana Barani Afrika, pamoja na kupanua mahusiano ya kitamaduni, kibiashara, na uwekezaji kati ya mabara yetu mawili."
Síkela naye alisema:
"Kwa kushirikiana na CAF, tunafanya ushirikiano wa Ulaya na Afrika kuwa dhahiri zaidi, wa kweli zaidi, na wa maana zaidi – hasa kwa vijana."
"Kipengele muhimu cha makubaliano haya ni msaada kwa Mashindano ya Soka ya Shule za Afrika yanayoandaliwa na CAF, ambayo yatafikia hadi shule 33,000 kote barani Afrika."
Makubaliano haya mapya ni sehemu ya mpango wa uwekezaji wa Global Gateway Africa-Europe. Kupitia mpango huu, Umoja wa Ulaya umeahidi kuwekeza angalau €150 bilioni (zaidi ya trilioni 400 za Shilingi za Tanzania) barani Afrika ifikapo mwaka 2027. Maeneo mengine ya uwekezaji wa Ulaya barani Afrika ni pamoja na mpito wa nishati safi na huduma za afya.
Uwekaji saini wa makubaliano haya pia unafanyika wakati mabara haya mawili yakisherehekea miaka 25 tangu kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika Cairo mwaka 2000.
Comments
Post a Comment