Ousmane Sonko awataka viongozi wa Afrika kusimamia uhuru wao wa kitaifa
Waziri Mkuu wa Senegal, Ousmane Sonko, ametangaza rasmi kuwa wanajeshi wote wa kigeni waliopo nchini humo wanapaswa kuondoka ifikapo mwisho wa mwezi Julai.
Kwa sasa, vikosi vya Ufaransa ndivyo pekee vya kigeni vilivyopo Senegal, vikifanya kazi chini ya makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi ya mwaka 2012. Katika hatua ya kuondoka kwa awamu, Ufaransa ilikabidhi rasmi kambi ya jeshi la majini ya Rear Admiral Protet iliyopo Dakar kwa mamlaka za Senegal mnamo Mei 15, ikifuatiwa na makabidhiano ya kambi za Marshall na Saint-Exupéry mwezi Machi. Kambi zilizobaki zinatarajiwa kukabidhiwa katika awamu zinazofuata.
Akizungumza na runinga ya taifa ya Burkina Faso (RTB) siku ya Jumatatu, Sonko alisema kuwa tangu serikali yake iingie madarakani takriban mwaka mmoja uliopita, imechukua hatua mbalimbali kudhibiti na kuimarisha mamlaka kamili ya taifa.
“Tumejulisha nchi zote zenye majeshi nchini Senegal kwamba tunataka waondoke kabisa. Hatutakuwa tena na kambi za kijeshi za kigeni katika ardhi ya Senegal,” Sonko alisisitiza.
Hatua hii ni sehemu ya mwelekeo mpana unaoshuhudiwa Afrika Magharibi, ambapo mataifa kama Burkina Faso, Mali, na Niger yamefukuza majeshi ya kigeni – hasa ya Ufaransa – kama ishara ya kujinasua kutoka ushawishi wa zamani wa kikoloni na kudhibiti mustakabali wao wa kiusalama na kisiasa.
Waziri Mkuu wa Senegal, Ousmane Sonko, amethibitisha kuwa mchakato wa kuondoa majeshi ya kigeni unaendelea kwa kasi. Alisema moja ya kambi za kijeshi za kigeni ilikabidhiwa rasmi siku mbili kabla ya mahojiano na akaongeza kuwa makabidhiano ya kambi nyingine yatafanyika ifikapo mwisho wa mwezi Julai.
Sonko alielezea hatua hiyo kama sehemu ya kudhibitisha mamlaka ya kitaifa, akisisitiza kuwa Senegal ina jeshi la taifa pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama, na kuamini nchi hiyo ina uwezo wa kulinda usalama wake wenyewe. Aidha, aliwahimiza viongozi wa mataifa mengine ya Afrika kuchukua hatua za kudhibiti hatima zao wenyewe kwa nguvu zaidi.
Mnamo Novemba 2023, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, alielezea uwepo wa majeshi ya Ufaransa nchini kama jambo lisilolingana na mamlaka ya taifa. Serikali yake mpya imechukua msimamo thabiti wa kupunguza uwepo wa kijeshi wa Ufaransa nchini.
Nchi kadhaa za Afrika Magharibi, ikiwa ni pamoja na Burkina Faso, Mali, na Niger, zimekatisha uhusiano wa kijeshi na Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni, zikitaja kushindwa kuridhika na juhudi za Ufaransa za kupambana na ugaidi na kuonyesha nia ya kutafuta washirika mbadala kama Russia.
Comments
Post a Comment