Rais wa Tanzania atoa onyo kwa wanaharakati wa Kenya wanaojihusisha na mambo ya ndani ya nchi

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewaonya wanaharakati kutoka nchi jirani ya Kenya kwamba hatawaruhusu "kuingilia" mambo ya ndani ya nchi yake na kusababisha "vurugu".

Kauli yake imekuja baada ya wanasheria maarufu wa Kenya na wanaharakati wa haki za binadamu kufukuzwa nchini, hali iliyowazuia kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini.

"Kama wameweza kudhibitiwa kwao, basi wasije hapa kuingilia. Tusiwape nafasi. Tayari wameshasababisha vurugu katika nchi yao," alisema Rais Samia.

Makundi ya haki za binadamu yameeleza wasiwasi kwamba serikali ya Tanzania inazidi kuwakandamiza wapinzani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.

Jumatatu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, Tundu Lissu, alifikishwa katika mahakama ya mwanzo baada ya kukamatwa mwezi uliopita.

Akiwa mahakamani, Lissu alinyanyua ngumi juu kama ishara ya kupinga na kudumu katika harakati, na kuwaambia wafuasi wake: "Mtakuwa salama. Msikubali kuishi kwa hofu."

Kulikuwa na ulinzi mkali wa vyombo vya usalama katika mahakama hiyo jijini Dar es Salaam, jiji kubwa zaidi nchini.

Hata hivyo, hilo halikuwazuia wafuasi wake, mamia kati yao walikusanyika nje ya mahakama kumuunga mkono.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 2 Juni baada ya upande wa mashtaka kuomba muda zaidi kwa ajili ya uchunguzi.

Awali, mahakama ilijaribu kuendesha kesi hiyo kwa njia ya mtandao (virtually), lakini timu ya mawakili wa Lissu ilipinga wakisema kuwa uwazi wa mchakato unahitajika.

Lissu alikamatwa tarehe 9 Aprili, baada ya kutoa wito maarufu wa "Hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi".

Anasisitiza kwamba sheria za sasa nchini Tanzania haziruhusu uchaguzi huru na wa haki. Serikali imekanusha madai hayo.

Baada ya kukamatwa, amefunguliwa mashtaka ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, zinazodaiwa kuchochea uasi na kuishutumu polisi kwa ubadhirifu wa uchaguzi.

Lissu amekana mashtaka yote. Ikiwa atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Timu ya mawakili wa Tundu Lissu imeeleza wasiwasi kuhusu uwepo mkubwa wa polisi waliokuwa wamezingira mahakama, jambo ambalo hakimu alilikubali na kusema kutakuwa na mashauriano kuhusu kama hatua hiyo ilikuwa na msingi wa kisheria.

Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kusifiwa sana kwa kuipa Tanzania nafasi kubwa ya uhuru wa kisiasa alipoingia madarakani mwaka 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa rais, John Magufuli.

Hata hivyo, wakosoaji wake sasa wanasema Tanzania inarudia enzi za ukandamizaji zilizokuwa maarufu wakati wa utawala wa Magufuli — jambo ambalo serikali inakanusha.

Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesema kuwa mwanaharakati kutoka Kenya, Boniface Mwangi, na wakili kutoka Uganda, Agather Atuhaire, walikamatwa walipowasili kuhudhuria kesi ya Lissu.

Msemaji mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, alisema hakuwa na taarifa za kukamatwa kwao, lakini angechunguza suala hilo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Jumapili, aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria wa Kenya, Martha Karua, alifukuzwa nchini Tanzania pamoja na wenzake wawili ili kuzuia kushiriki kwenye kesi ya Lissu.

Masaa machache baadaye, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, Willy Mutunga, pamoja na wanaharakati wengine mashuhuri wa haki za binadamu, walizuiliwa uwanja wa ndege.

Hata hivyo, aliyekuwa Jaji Mkuu mwingine wa Kenya, David Maraga, aliruhusiwa kufika mahakamani, ambapo alieleza matumaini yake kwamba mchakato wa kisheria utakuwa wa haki, wazi, na wa haraka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa sera mpya ya mambo ya nje ya Tanzania jijini Dar es Salaam, siku ya Jumatatu, Rais Samia alisisitiza kuwa hatavumilia juhudi zozote kutoka nje zinazolenga kuhatarisha amani na utulivu wa nchi yake.

"Hatutaruhusu mtu yeyote aje kutuharibu," alisema.

Aliagiza mamlaka kuhakikisha kwamba "wale waliovuruga nchi zao wasivuke kuja Tanzania... na kueneza tabia zao za utovu wa nidhamu hapa."

"Nimeona video kadhaa zikinishutumu kuwa ninapendelea, lakini ninachofanya ni kulinda nchi yangu – jukumu kuu nililopewa," aliongeza.

Matukio ya hivi karibuni Tanzania — ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa viongozi wengine wa upinzani, pamoja na wimbi la utekaji na mauaji dhidi ya wakosoaji wa serikali — yamezua kulaaniwa kimataifa na wito wa kusitisha ukandamizaji wa kisiasa.

Chama cha Chadema kimeondolewa kushiriki uchaguzi mkuu ujao, baada ya kukataa kusaini kanuni ya maadili iliyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Comments