New York Times imedai kwamba Elon Musk amekuwa akitumia dawa za kulevya kupita kiasi na ana utegemezi wa dawa hizo, ikiwemo ketamini na dawa nyingine za kusisimua akili.
Mshauri wa Rais wa Marekani, Donald Trump, anaripotiwa kutumia kwa wingi ketamini na dawa nyingine za kulevya, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.
Bilionea wa teknolojia Elon Musk, ambaye ni mshirika mkubwa wa Rais wa Marekani Donald Trump, anaripotiwa kutumia dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa na cha kutisha, kwa mujibu wa New York Times.
Ripoti hiyo ilitolewa muda mfupi baada ya Musk kutangaza kujiuzulu kutoka uongozi wa Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE), ambayo ilikuwa na jukumu la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya serikali ya Marekani.
Ingawa awali Musk alikiri kutumia ketamini mara moja kila wiki mbili kwa ajili ya msongo wa mawazo, New York Times inadai kwamba sasa amekuwa na uraibu mkubwa zaidi, akitumia ketamini mara kwa mara—wakati mwingine kila siku—na kuichanganya na dawa nyingine kama ecstasy na uyoga wa kiakili (psychedelic mushrooms).
Kwa mujibu wa New York Times, Elon Musk anaripotiwa kusafiri na kisanduku cha dawa za kila siku chenye vidonge takriban 20, ikiwemo Adderall, dawa ya kusisimua akili inayotumika kutibu matatizo ya umakini (ADHD). Pia alishawahi kuonywa mapema kuhusu vipimo vya ghafla vya dawa kwa wafanyakazi wa SpaceX.
Mnamo 2018, The New York Times iliripoti kwamba baadhi ya wajumbe wa bodi ya Tesla walikuwa na wasiwasi kuhusu matumizi ya Musk ya dawa ya usingizi ya Ambien. Mwaka jana, Wall Street Journal iliripoti kwamba viongozi wakuu wa SpaceX na Tesla walieleza wasiwasi juu ya matumizi yake ya dawa nyingine, ikiwemo LSD na kokeini.
Katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu ya Marekani akiwa na Trump, Musk aliepuka kujibu moja kwa moja swali kuhusu madai ya matumizi ya dawa, na akikosoa New York Times kwa kuwa ni “gazeti lilelile lililopewa tuzo ya Pulitzer kwa ripoti ya uongo kuhusu Russiagate.”
Musk alisema mwaka 2024 kwamba vipimo vya mwili vilivyofanywa kwa miaka mitatu kwenye SpaceX havikuonyesha hata chembe ya dawa au pombe.
Aliongeza kuwa kuondoka kwake DOGE (Idara ya Ufanisi wa Serikali) “siyo mwisho wa DOGE,” na atabaki kuwa mshauri na rafiki wa Rais Trump.
Comments
Post a Comment