Musk anajiuzulu kama mfanyakazi maalum wa serikali.

Tajiri wa teknolojia ameongoza kikosi kazi cha DOGE kinacholenga kupunguza matumizi ya serikali.


Tajiri wa teknolojia Elon Musk, mkuu wa Idara ya Ufanisi wa Serikali ya Marekani (DOGE), ametangaza kuwa hatatumika tena kama mfanyakazi wa serikali.

Tangazo hilo linakuja huku kukiwa na taarifa za kuwepo kwa mvutano unaokua kati ya Musk na Rais Donald Trump.

Trump alianzisha DOGE kwa lengo la kubaini na kuondoa matumizi mabaya ya fedha za umma, kama sehemu ya juhudi za kulifanya serikali ya shirikisho kuwahudumia wananchi wa kawaida kwa ufanisi zaidi.

Chini ya uongozi wa Musk, DOGE imeondoa ruzuku na miradi mbalimbali ya serikali, na pia kufuta baadhi ya nafasi za kazi. Trump pia alilitumia shirika hilo kuvunja Idara ya Elimu na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa X, Musk aliandika Jumatano jioni:

"Kwa kuwa muda wangu kama Mfanyakazi Maalum wa Serikali unakaribia mwisho, ningependa kumshukuru Rais Trump kwa kunipa fursa ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima."

Musk asema juhudi za DOGE zitaendelea kuimarika, licha ya kuondoka kwake serikalini

Elon Musk amesema kuwa,

“Dhamira ya DOGE itaendelea kuimarika kadri inavyozoeleka kama mtindo wa maisha katika serikali.”

Gazeti la New York Times limeeleza kuwa wafanyakazi maalum wa serikali huajiriwa kwa ajili ya kazi muhimu lakini maalum, kwa muda usiozidi siku 130, na wanaweza kulipwa au kufanya kazi bila malipo.

Afisa mmoja wa Ikulu ya Marekani (White House), ambaye hakutajwa jina, amethibitisha kwa shirika la habari la Reuters kwamba Musk anaondoka rasmi kwenye utawala, na taratibu za kuachia wadhifa wake zimeanza Jumatano usiku.

Musk hivi karibuni alieleza kukatishwa tamaa na mswada wa kodi na matumizi ya fedha wa Trump, akisema utaongeza nakisi ya bajeti na kudhoofisha lengo la DOGE la kupunguza matumizi. Wiki iliyopita, Musk alisema pia anapanga kuachana na siasa, kwa sababu anahisi "ameshafanya vya kutosha."

Rais Trump ametetea mswada huo wa kodi uliopitishwa na Bunge wiki iliyopita, lakini alieleza kuwa kuna vipengele fulani ambavyo "havampendezi."

Kwa mujibu wa tovuti ya DOGE, kikosi kazi hicho kimeokoa takriban dola bilioni 175 kutoka kwa walipa kodi. Hata hivyo, Democrats wamekosoa mpango huo, na baadhi ya hatua zake zimezuiwa na mahakama. 

Comments