Migodi ya koltani inayodhibitiwa na waasi nchini Kongo inaendelea kusambaza madini kwa ajili ya teknolojia ya dunia.


Katika vilima vya kijani vya Masisi, jimboni Kivu Kaskazini, shughuli katika machimbo ya Rubaya zinaendelea kwa kishindo huku jenereta zikipiga kelele, na vumbi jeupe likitapakaa kote kwenye mandhari.

Maelfu ya wafanyakazi wanachimba kwa mikono yao madini muhimu kama vile koltani, kasiteriti, na manganisi — ambayo ni ya lazima kwa utengenezaji wa simu, betri, na teknolojia nyingine za kisasa.

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikikumbwa na migogoro kwa miongo kadhaa, ikiwa na zaidi ya makundi 100 ya waasi, mengi yao yakipigania maeneo ya madini karibu na mpaka wa Rwanda.

Mgogoro huu umechangia katika moja ya maafa makubwa ya kibinadamu duniani, ambapo zaidi ya watu milioni 7 wamelazimika kuhama makazi yao — wakiwemo 100,000 waliokimbia mwaka huu pekee.

Mgodi wa Rubaya na maeneo ya jirani uko chini ya udhibiti wa kundi la waasi la M23.

Migodi kama hii imekuwa kiini cha mijadala kuhusu M23 kutwaa sehemu ya mashariki ya Kongo, ambapo serikali ya Kongo inadai kundi hilo linataka kudhibiti madini na kuyasafirisha kinyume cha sheria kwenda Rwanda.

Kwa wanaume wanaofanya kazi katika migodi ya Rubaya, hali haijabadilika sana — ingawa baadhi yao wanasema hali ya kazi ni nafuu zaidi chini ya waasi.

Jean Baptiste Bigirimana, ambaye amefanya kazi migodini kwa miaka saba, alisema:

“Ninapata dola 40 kwa mwezi, lakini hiyo haitoshi. Watoto wanahitaji nguo, elimu, na chakula. Nikigawanya hiyo pesa, siwezi kuwatunza vizuri,” alisema, akiongeza kuwa hajui madini anayochimba hupelekwa wapi yakiondoka Rubaya.

Wakati mwingine, migodi hiyo pia ilikuwa chini ya udhibiti wa Wazalendo, kundi la kijeshi linaloshirikiana na jeshi la Kongo.

Alexis Twagira, ambaye amefanya kazi mgodini kwa miaka 13, alisema baadhi ya mambo yameboreshwa chini ya M23:

“Wakati wa Wazalendo, walikuwa wanatunyanyasa, wakati mwingine kutuchukulia madini yetu na kutulazimisha kutoa fedha,” alisema.

Mwezi Aprili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisimamia kutiwa saini kwa makubaliano kati ya Kongo na Rwanda ya kutafuta amani katika eneo hilo, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa madini ya mashariki ya Kongo kwa Marekani.

Rais wa Kongo Félix Tshisekedi alitafuta makubaliano na utawala wa Trump ili kutoa upendeleo kwa Marekani kupata rasilimali za Kongo kwa urahisi zaidi, kwa masharti kwamba Marekani ingesaidia kupunguza mivutano na machafuko.

Kongo na Rwanda wanatumaini kuwa ushiriki wa Marekani — pamoja na uwekezaji mkubwa endapo kutakuwepo na usalama wa kutosha kwa kampuni za Kimarekani kufanya kazi — utaweza kupunguza mapigano na ukatili wa makundi ya waasi ambao umeshindikana kudhibitiwa tangu miaka ya 1990.

Bahati Moïse, mfanyabiashara anayesafirisha koltani kutoka migodi ya Rubaya, alisema anatumaini wafanyakazi wa migodini wataheshimiwa kama madini wanayochimba kwa juhudi kubwa.

“Nchi nzima, dunia nzima inajua kuwa simu zinatengenezwa kwa koltani inayotoka hapa, lakini angalia maisha tunayoyaishi,” alisema.

“Hatuwezi kuendelea hivi.”

Comments