"Inaripotiwa kuwa mkuu wa usalama wa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ameuwawa."
Mapigano ya silaha yalizuka katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, jioni ya Jumatatu kufuatia taarifa za kuuawa kwa kamanda mwandamizi wa kijeshi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Al Jazeera, Abdul Ghani al-Kikli, aliyekuwa mkuu wa Kikosi cha Usaidizi wa Utulivu (Stability Support Apparatus – SSA) cha serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, aliuawa katika mapigano ya risasi kusini mwa Tripoli. Tukio hilo liliripotiwa kutokea ndani ya makao makuu ya Brigedi ya Mapambano ya 444, baada ya “mazungumzo yaliyogonga mwamba.”
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti mapigano na harakati za wanajeshi katika maeneo ya Abu Salim na Mashrou. Al Jazeera ilinukuu mashuhuda wakisema kwamba wanajeshi kutoka brigedi ya 111 na 444 walivamia makao makuu ya SSA, huku milio ya risasi na milipuko ikisikika katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Bado haijafahamika wazi kiwango cha mapigano na idadi kamili ya waathirika. Picha za kutisha zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha miili kadhaa. Al Jazeera iliripoti kuwa angalau watu sita wamejeruhiwa.
Kwa mujibu wa Al Arabiya, wanamgambo kutoka Misrata na miji mingine walianza kuelekea Tripoli wiki iliyopita.
SSA ilianzishwa mwaka 2021 na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa lengo la kulinda usalama wa mji mkuu na kupambana na uhalifu uliopangwa.
Umoja wa Mataifa wataka hali ya utulivu irejee Tripoli
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi nchini Libya (UNSMIL) umesema kuwa unafuatilia kwa karibu taarifa za kuongezeka kwa majeshi na mvutano unaoendelea katika mji wa Tripoli na maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo.
“Tunaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa za mkusanyiko wa kijeshi na ongezeko la mvutano katika Tripoli na eneo pana la magharibi,” ilisema taarifa ya UNSMIL.
“Tunaendelea kusisitiza kwa dharura kuwa pande zote zichukue hatua za haraka kutuliza hali ya sasa, zue vitendo vyovyote vya uchokozi, na kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo,” ujumbe huo uliongeza.
Libya iliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kupinduliwa kwa Gaddafi
Libya iliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011 baada ya maandamano yaliyoungwa mkono na NATO, yaliyosababisha kuuawa kwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Mapigano hayo hatimaye yaliibua mgawanyiko kati ya serikali pinzani – moja ikiwa na makao yake Tripoli, magharibi mwa nchi, na nyingine Tobruk, mashariki mwa Libya.
Mapigano makubwa ya mwisho kati ya makundi ya wanamgambo mjini Tripoli yalitokea Agosti 2023, ambapo watu 55 waliuawa na takribani wengine 150 kujeruhiwa.
Mnamo Februari 2025, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Masuala ya Baraza la Mawaziri, Adel Juma, alinusurika jaribio la kutaka kumuua.
Comments
Post a Comment