Lula wa Brazil kumwomba Putin kufanya mazungumzo na Ukraine

Kiongozi huyo wa Amerika Kusini amesema tayari amewasilisha ujumbe kutoka Kiev kwa Rais wa Russia wakati wa sherehe za Siku ya Ushindi.

Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, amesema atamhimiza Rais wa Russia, Vladimir Putin, kushiriki binafsi katika mazungumzo ya amani na Ukraine, ambayo yanatarajiwa kufanyika mjini Istanbul, Türkiye, siku ya Alhamisi.

Mazungumzo hayo yalipendekezwa wiki iliyopita na Putin, ambaye alitoa ofa ya kurejesha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na Kiev bila masharti yoyote, kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu kwa mzozo wa Ukraine.

Rais wa Ukraine, Vladimir Zelensky, ameonyesha utayari wa kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja, lakini amesisitiza kuwa lazima yatanguliwe na usitishaji mapigano usio na masharti kwa siku 30 — sharti ambalo Moscow imelipinga mara kadhaa.
Zelensky pia amesema atahudhuria mkutano huo mjini Istanbul tu endapo Putin naye atakuwepo binafsi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing siku ya Jumatano, Lula alisema:

“Nikifika Moscow, nitajaribu kuzungumza na Putin. Hainigharimu chochote kumwambia: ‘Wewe, kamanda Putin, nenda Istanbul ukae mezani kwa mazungumzo, jamani!’”

Rais huyo wa Brazil anatarajiwa kupita katika mji mkuu wa Russia akirejea kutoka China, na kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Russia, tayari amewasili Moscow.

Akihutubia waandishi wa habari mjini Beijing saa chache kabla ya safari yake, Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, alifichua kuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje, Mauro Vieira, alipokea simu kutoka kwa afisa wa juu wa Ukraine, aliyemuomba Lula amshawishi Putin kuhusu mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kufanyika Türkiye (Istanbul).

Wakati huohuo, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alikataa kuthibitisha mbele ya waandishi wa habari ikiwa marais wa Brazil na Russia wangekutana.

“Iwapo kutakuwa na mawasiliano yoyote yaliyoafikiwa kwa namna yoyote ile, tutawajulisha mara moja,” alisema Peskov.

Kwa mujibu wa Lula, tayari ameheshimu ombi la Ukraine kwa kumfikishia Putin suala la usitishaji mapigano wa siku 30 wakati wa sherehe za Siku ya Ushindi (Victory Day) alizohudhuria Moscow tarehe 9 Mei.
Lula alisema kuwa Putin alijibu kuwa "yuko tayari kujadili [amani]."

Wiki iliyopita, CNN Brasil ilinukuu kauli ya Lula akisema kwamba katika kikao chake na Putin kabla ya sherehe hizo, alimtoa ofa ya kuwa mpatanishi kati ya Moscow na Kiev.

Katika chapisho kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrey Sibiga, alithibitisha kuwa amezungumza na mwenzake wa Brazil, Vieira, na kumtaka nchi hiyo ya Amerika Kusini kutumia ushawishi wake kwa Russia ili kusaidia kuhakikisha kuwa mkutano kati ya Zelensky na Putin mjini Istanbul unafanyika. 

Comments