Kapteni Ibrahim Traoré, mwenye umri wa miaka 37 na kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, amejijengea taswira ya kiongozi wa Kiafrika mwenye msimamo wa kupinga ubeberu wa Magharibi na ukoloni mamboleo. Ujumbe wake wa kujitegemea na kupigania uhuru wa kweli wa bara la Afrika umevutia watu wengi barani na duniani.
Wengi wanamfananisha na shujaa wa zamani wa Burkina Faso, Thomas Sankara, aliyekuwa mzalendo na mwanamapinduzi wa Ki-Marxist. Traoré aliposhika madaraka kwa mapinduzi mwaka 2022, aliachana na ushawishi wa Ufaransa na kuanzisha ushirikiano wa karibu na Urusi. Alianzisha sera za kiuchumi za mrengo wa kushoto, kama vile kuunda kampuni ya taifa ya madini na kulazimisha makampuni ya kigeni kutoa asilimia 15 ya hisa kwa serikali na kuwajengea Waburkina ujuzi.
Ujumbe wake wa kizalendo na kupigania haki za Afrika unaendelea kuungwa mkono na watu wengi, hasa vijana wanaotilia shaka uhusiano wa sasa kati ya Afrika na mataifa ya Magharibi huku bara likisalia maskini licha ya rasilimali lukuki.
Sheria hiyo ilimhusu pia mchimbaji wa dhahabu kutoka Urusi, Nordgold, ambaye alipatiwa leseni mwishoni mwa Aprili kwa ajili ya uwekezaji wake mpya katika sekta ya dhahabu ya Burkina Faso.
Kama sehemu ya kile ambacho Kapteni Traoré anakitaja kuwa ni “mapinduzi” ya kuhakikisha taifa linanufaika na utajiri wake wa madini, utawala wake wa kijeshi unajenga kiwanda cha kusafisha dhahabu na kuanzisha akiba ya dhahabu ya taifa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.
Hata hivyo, kampuni zinazomilikiwa na mataifa ya Magharibi zinaonekana kukumbwa na wakati mgumu. Kampuni ya Sarama Resources yenye makao yake makuu Australia, ilianzisha mchakato wa usuluhishi dhidi ya Burkina Faso mwishoni mwa 2024 baada ya leseni ya utafiti kufutwa.
Junta pia imetaifisha migodi miwili ya dhahabu iliyokuwa inamilikiwa na kampuni iliyoorodheshwa katika soko la hisa la London, na mwezi uliopita ilitangaza mpango wa kuchukua udhibiti wa migodi mingine inayomilikiwa na wageni.
Enoch Randy Aikins, mtafiti kutoka Taasisi ya Masuala ya Usalama ya Afrika Kusini, aliambia BBC kuwa mageuzi haya makubwa yameongeza umaarufu wa Traoré barani Afrika.
“Kwa sasa, huenda ndiye rais maarufu zaidi barani Afrika – au hata kipenzi cha watu,” alisema Aikins.
Umaarufu wa Kapteni Ibrahim Traoré umechochewa sana kupitia mitandao ya kijamii, ingawa mara nyingi kupitia machapisho yenye upotoshaji yanayolenga kuimarisha taswira yake ya kimapinduzi.
Video zilizotengenezwa kwa kutumia akili bandia (AI) zimeonyesha wasanii maarufu kama R Kelly, Rihanna, Justin Bieber na Beyoncé wakimuimbia Traoré – ingawa kwa hakika hawajafanya hivyo.
Bi Beverly Ochieng alisema Traoré alianza kuvuta macho ya Waafrika alipohutubia mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika mwaka 2023, ambapo aliwataka viongozi wa Afrika “waache kuwa vikaragosi wanaocheza kila wakati wakoloni wanapovuta nyuzi.”
Hotuba hiyo ilisambazwa sana na vyombo vya habari vya Urusi, ambavyo vina jukumu kubwa katika kukuza taswira yake ya kupinga ubeberu.
Wiki iliyopita, Traoré alihudhuria maadhimisho ya miaka 80 ya ushindi wa Umoja wa Kisovyeti dhidi ya Nazi wa Ujerumani, na akaandika kwenye X kwamba yeye pamoja na viongozi wa kijeshi wa Mali na Niger wamepata msukumo wa “kushinda vita dhidi ya ugaidi na ubeberu kwa gharama yoyote.”
Kupitia hotuba zake kali na kampeni makini ya mitandaoni, Traoré amepata wafuasi hata nje ya Afrika – akiwemo miongoni mwa Wamarekani Weusi na Waingereza Weusi. Bi Ochieng alisema: “Kila mtu aliyeathiriwa na ubaguzi wa rangi, ukoloni au utumwa anaweza kujihusisha na ujumbe wake.”
Rapa Meek Mill wa Marekani aliwahi kumpongeza kwenye X, akisema anavutiwa na “nguvu na moyo” wake – japokuwa alikejeliwa baada ya kumchanganya jina na kuiita “Burkina Faso,” kabla ya kufuta chapisho hilo.
Lakini Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, si mpenzi wake. Alimtaja Traoré kuwa sehemu ya “muungano wa ajabu kati ya wanaojiita waafrika halisi na mabeberu wapya,” akimaanisha Urusi na China. Macron amewalaumu kwa kuchochea mapinduzi katika koloni za zamani za Ufaransa Afrika na kutumia unafiki katika mijadala ya ukoloni na uhuru wa kweli.
Licha ya umaarufu wake, Traoré hajatimiza ahadi yake ya kumaliza uasi wa Kiislamu uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 na kuleta migawanyiko ya kikabila, ambao sasa umeenea hadi mataifa jirani yaliyokuwa na amani kama Benin.
Pia utawala wake umekuwa ukikandamiza upinzani, vyombo vya habari, na mashirika ya kiraia – huku wakosoaji wakitumikishwa kwa nguvu katika medani ya vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu.
Kwa Rinaldo Depagne, naibu mkurugenzi wa Afrika katika taasisi ya utafiti ya International Crisis Group, Kapteni Ibrahim Traoré anapata uungwaji mkono mkubwa kwa sababu “ni kijana katika nchi yenye idadi kubwa ya vijana” – ambapo wastani wa umri ni miaka 17.7.
“Anajua kutumia vyombo vya habari, na anatumia historia kujijengea umaarufu kama mwendelezo wa Thomas Sankara,” aliambia BBC.
“Na anauelewa mchezo wa siasa – jinsi ya kuifanya nchi iliyojeruhiwa sana na vita kuamini kuwa kuna kesho bora. Anauelewa sana huo mchezo.”
Sankara alipata madaraka kupitia mapinduzi mwaka 1983 akiwa na miaka 33, na akaiunganisha nchi kwa kauli mbiu: “Nchi au kifo, tutashinda!” Alikufa miaka minne baadaye kwenye mapinduzi mengine yaliyoirudisha Burkina Faso katika ushawishi wa kisiasa wa Ufaransa hadi Traoré alipochukua madaraka.
Profesa Kwesi Aning, mchambuzi wa usalama kutoka Ghana ambaye aliwahi kufanya kazi katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Kimataifa cha Kofi Annan, alisema umaarufu wa Traoré unaashiria mabadiliko ya kisiasa barani Afrika, hasa Afrika Magharibi.
Utafiti wa mwaka 2024 wa Afrobarometer katika nchi 39 ulionyesha kushuka kwa uungwaji mkono kwa demokrasia, ingawa bado ndiyo mfumo wa serikali unaopendwa zaidi.
“Demokrasia imeshindwa kuleta matumaini kwa vijana. Haijatoa ajira, wala elimu na huduma bora za afya,” Prof Aning aliambia BBC.
Alisema Traoré “anatoa mbadala, na anafufua roho ya vipindi viwili vya kihistoria”:
-
Kipindi cha baada ya uhuru, ambacho kilikuwa na viongozi kama Kwame Nkrumah wa Ghana na Kenneth Kaunda wa Zambia.
-
Na kipindi cha baadaye kilichokuwa na viongozi kama Thomas Sankara na Jerry Rawlings wa Ghana, ambaye mapinduzi yake ya mwaka 1979 “yalikuwa maarufu sana wakati huu"
Ni Kapteni Ibrahim Traoré aliyeiba shoo wakati wa kuapishwa kwa Rais wa Ghana, John Mahama, mwezi Januari, alipowasili akiwa amevaa sare za kivita na bastola kiunoni.
“Japo tayari kulikuwa na marais 21 wa nchi mbalimbali, Traoré alipoingia tu, ukumbi ulilipuka kwa shangwe. Hata walinzi wa rais wangu walikuwa wanamkimbilia,” alisema Profesa Kwesi Aning.
Prof. Aning alieleza kuwa Traoré alionekana tofauti kabisa na baadhi ya viongozi wa Afrika waliokuwa wakihangaika kutembea lakini bado wameshikilia madaraka kwa njia za wizi wa kura.
“Traoré ana mvuto na kujiamini, uso wake huwa wazi na huvaa tabasamu dogo. Ni mzungumzaji mzuri pia, na hujitambulisha kama mtu wa kawaida,” aliongeza.
Licha ya kuwa na uhusiano wa karibu na Urusi, utawala wake umeonesha maendeleo ya kiuchumi. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia vilitoa tathmini nzuri mapema Aprili:
-
IMF ilisema kuwa licha ya changamoto za kibinadamu na kiusalama, uchumi wa Burkina Faso unatarajiwa kubaki imara mwaka 2025. Pia walitaja mafanikio katika ukusanyaji mapato ya ndani, kudhibiti mishahara ya umma, na kuongeza bajeti ya elimu, afya, na ulinzi wa jamii.
-
Benki ya Dunia iliripoti kuwa mfumuko wa bei umeongezeka kutoka 0.7% mwaka 2023 hadi 4.2% mwaka 2024, lakini kiwango cha umaskini uliokithiri (wanaoishi kwa chini ya $2.15 kwa siku) kilipungua hadi 24.9% kutokana na ukuaji mzuri katika sekta ya kilimo na huduma.
Hata hivyo, uhusiano na Ufaransa na Marekani umekuwa wa mashaka. Mfano wa hivi karibuni ni madai ya Jenerali Michael Langley wa Jeshi la Marekani barani Afrika, aliyesema kuwa Traoré anatumia hifadhi ya dhahabu ya taifa kwa manufaa ya utawala wake badala ya maslahi ya wananchi.
Kauli hiyo inaashiria mtazamo wa muda mrefu wa Marekani na baadhi ya washirika wake Afrika kwamba Urusi inamlinda Traoré kwa mkataba wa kupata dhahabu ya Burkina Faso – jambo linalopingana na taswira ya Traoré kama shujaa aliyewafukuza wanajeshi wa Ufaransa mwaka 2023 ili kurudisha mamlaka ya kitaifa.
Matamshi hayo ya Langley yaliyotolewa mbele ya kamati ya Seneti ya Marekani, yaliibua hasira kubwa kwa wafuasi wa Traoré, waliodai kuwa shujaa wao anachafuliwa.
Hasira hizo ziliongezeka zaidi baada ya junta ya Burkina Faso kutangaza kuwa imezuia jaribio la mapinduzi, ikidai kuwa waliopanga njama hiyo walikuwa nchini Ivory Coast – ambako ndipo Jenerali Langley alipozuru siku chache baadaye.
Hata hivyo, junta ilichukua fursa hii kuandaa moja ya mikutano yake mikubwa zaidi katika mji mkuu wa Burkina Faso kwa hofu kwamba "mabeberu" na "wasaidizi wao" walikuwa wanajaribu kumng'oa kapteni.
"Kwa sababu Colin Powell alidanganya, Iraq iliharibiwa. Barack Obama alidanganya, Gaddafi aliuawa. Lakini mara hii, uongo wao hautatuathiri," aliiambia Associated Press mchambuzi wa muziki, Ocibi Johann.
Mikutano ya mshikamano na Traoré iliandaliwa pia nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na London, siku hiyo hiyo.
Baada ya hapo, alitumia mitandao ya kijamii, akiandika kwa Kifaransa na Kiingereza, kutoa shukrani kwao kwa kushiriki maono yake "kwa Burkina Faso mpya na Afrika mpya," akiongeza: "Pamoja, kwa mshikamano, tutashinda mabeberu na ukoloni mpya kwa Afrika huru, yenye heshima na yenye uhuru."
Hawezi kusemwa ni vipi mambo yatakwenda kwa kapteni mdogo, lakini yeye - pamoja na viongozi wa kijeshi huko Mali na Niger - wameleta mabadiliko makubwa huko Magharibi mwa Afrika, na nchi nyingine zimefuata mfano wao kwa kuamuru vikosi vya Ufaransa kuondoka.
Nchi hizi tatu zinazotawala kijeshi pia zimejiondoa katika umoja wa kibiashara na usalama wa kikanda ECOWAS, zimeunda muungano wao wenyewe, na kumaliza biashara ya bure katika kanda kwa kutangaza kuanzisha ushuru wa 0.5% kwa bidhaa zinazokuja katika nchi zao.
Bwana Aikins alisema kuwa Traoré anaweza kujifunza kutoka kwa wengine, akionyesha kwamba wakati Jerry Rawlings alipopata madaraka huko Ghana akiwa na umri wa miaka 32, alijulikana kama "Junior Jesus" lakini baada ya miaka 19 aliondoka na urithi mchanganyiko - alishindwa kukomesha rushwa licha ya kusaidia kuunda demokrasia "inayodumu."
Kwa "urithi wa kudumu," Bwana Aikins alisema, Traoré anapaswa kuzingatia kufikia amani na kujenga taasisi imara za serikali ili kuleta utawala bora badala ya "kufanya madaraka kuwa yake binafsi" na kudhibiti upinzani.
-
Ivory Coast ilikanusha kuhusika katika njama yoyote, huku US Africa Command ikisema kuwa ziara ya Jenerali Langley ilikuwa imelenga kushughulikia "changamoto za usalama za pamoja," ikijumuisha "itikadi kali za kigaidi."
Comments
Post a Comment