Kiongozi wa Afrika Aliyetimuliwa Ahama Nchi, Aelekea Nchi Jirani

Ali Bongo na familia yake wameondoka nchini Gabon na kuhamia Angola baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kufuatia mapinduzi ya Agosti 2023.


Rais Aliyetimuliwa wa Gabon, Ali Bongo, Aachiliwa na Kuhamia Angola

Rais wa zamani wa Gabon Ali Bongo na familia yake wameachiliwa kutoka kwenye kifungo cha nyumbani na kupelekwa Angola kwa ndege, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), João Lourenço, alitangaza siku ya Ijumaa.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Lourenço, ambaye pia ni Rais wa Angola, kutembelea nchi hiyo ya Afrika ya Kati na kufanya mazungumzo na kiongozi wa sasa Brice Oligui Nguema, aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 2023 yaliyomuondoa Bongo madarakani.

“Kutokana na juhudi za Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa wakati huu, João Lourenço, pamoja na Rais Brice Oligui Nguema wa Gabon, familia ya Bongo imeachiliwa na tayari imewasili Luanda,” ilisema taarifa kutoka Ikulu ya Angola iliyochapishwa kwenye Facebook.

Mke wa Bongo, Sylvia Bongo Ondimba, na mwana wao, Noureddin Bongo Valentin, walihamishwa kutoka gerezani hadi kifungo cha nyumbani wiki iliyopita, baada ya kuzuiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja wakikabiliwa na mashtaka ya ufisadi, utakatishaji fedha, na matumizi mabaya ya fedha za umma. Walihamishiwa katika makazi ya kifamilia mjini Libreville, mji mkuu wa Gabon, ambako Bongo alikuwa akiishi tangu kuondolewa kwake madarakani.

Vyombo vya habari vya ndani viliripoti awali kwamba mke wa zamani wa rais pamoja na mwanawe wako chini ya usimamizi wa kimahakama, na watahitajika kushirikiana na mamlaka za ndani wakati wakisubiri kesi yao kusikilizwa.

Sylvia Bongo alikamatwa rasmi mnamo Oktoba 2023, miezi kadhaa baada ya mapinduzi. Wakili wake aliwahi kuelezea kukamatwa kwake kama “kukatiliwa bila msingi” na “kinyume cha sheria.”

Familia ya Bongo imekuwa ikitawala siasa za Gabon kwa zaidi ya miongo mitano.
Ali Bongo alichukua uongozi mwaka 2009 kufuatia kifo cha baba yake, Omar Bongo, aliyekuwa rais tangu mwaka 1967. Urais wa Ali Bongo ulifikia kikomo mwezi Agosti 2023, baada ya Jenerali Brice Oligui Nguema kuongoza mapinduzi ya kijeshi kufuatia uchaguzi wenye utata.

Mamlaka ziliishtaki Sylvia Bongo kwa kumnyonya mumewe kisiasa kutokana na hali yake mbaya ya kiafya — alipatwa na kiharusi mwaka 2018 — na kufuja fedha za umma kwa kushirikiana na baadhi ya maafisa wakuu wa serikali.
Sylvia na mwanawe wamekanusha mashtaka hayo yote.

Rais wa zamani wa Gabon aliwahi kuanzisha mgomo wa kula mwaka jana kama njia ya kupinga madai ya unyanyasaji dhidi ya familia yake waliokuwa wakizuiliwa.

Mnamo Aprili 30, Umoja wa Afrika (AU) ulipitisha azimio lililotaka kuachiliwa kwa Bongo na familia yake, ukizitaka mamlaka mpya za koloni la zamani la Ufaransa kulinda haki na usalama wa familia hiyo.

Serikali ya Gabon haijatoa kauli rasmi kuhusu kile ambacho chombo cha habari cha ndani, Gabon Review, kilikitaja kama kuachiliwa kwa siri na kuhamishwa kwa familia ya Bongo kwenda Angola.

Rais Brice Oligui Nguema – ambaye alishinda uchaguzi wa mwezi uliopita kwa kura 90.35% – pia ni mpwa (au binamu) wa Ali Bongo.

Comments