Mashambulizi hayo, yaliyopewa jina la "Magari ya Vita ya Gideoni" (Gideon’s Chariots), yanaripotiwa kuwa na lengo la "kuiteka" kwa ukamilifu eneo lote la Wapalestina la Ukanda wa Gaza.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) latangaza kampeni mpya ya mabomu Gaza kwa lengo la kulishinda kundi la Hamas
Mashambulizi haya mapya yameanzishwa baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwa yamefadhiliwa na Marekani, Misri, na Qatar kumalizika mwezi Machi.
“Tangu jana, IDF imeendesha mashambulizi makubwa na kuhamasisha vikosi kuteka maeneo ya kimkakati katika Ukanda wa Gaza, kama sehemu ya hatua za awali za Operesheni Magari ya Vita ya Gideoni (Gideon’s Chariots) na upanuzi wa kampeni huko Gaza,” Jeshi la Israel lilisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa jioni.
IDF imesisitiza tena malengo yake ya kuwaokoa mateka waliobaki na “kulishinda kundi la Hamas.”
“Vikosi vya IDF chini ya Kamandi ya Kusini vitaendelea kuchukua hatua kulinda raia wa Israel na kutekeleza malengo ya vita,” jeshi hilo liliendelea.
Kwa mujibu wa Times of Israel, IDF inalenga “kuiteka” Gaza, kuwahamisha Wapalestina hadi sehemu ya kusini ya ukanda huo, na kuzuia “makundi ya kigaidi” kunyakua misaada ya kibinadamu.
Kulingana na Al Jazeera, takriban Wapalestina 115 wameuawa tangu alfajiri ya siku ya Ijumaa.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yalivunjika mwezi Machi baada ya pande zote kushindwa kuelewana juu ya utekelezaji wa awamu ya pili ya makubaliano hayo.
Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas kufuatia shambulio la ghafla lililofanywa na wanamgambo wa Kipalestina tarehe 7 Oktoba 2023, ambalo liliua takriban watu 1,200 na kupelekea watu zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka.
Tangu kuanza kwa mzozo huo, zaidi ya Wapalestina 53,000 wameuawa, na mashirika ya haki za binadamu yameishtumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari.
Comments
Post a Comment