Chris Brown aachiwa kwa dhamana ya pauni milioni 5 na mahakama ya London

Msanii wa Marekani Chris Brown aachiwa kwa dhamana na mahakama ya London baada ya kushtakiwa kwa "shambulio lisilo na kichocheo" katika kilabu cha usiku mwaka 2023.


Nyota huyo mshindi wa tuzo ya Grammy, ambaye bado hajaombwa kutoa maelezo ya kukubali au kukataa mashtaka hayo, sasa anaweza kuanza ziara yake ya kimataifa mwezi ujao kama ilivyopangwa, ikiwa ni sehemu ya masharti ya dhamana yake.

Alikamatwa wiki iliyopita na baadaye akashtakiwa kwa kosa la kusababisha madhara makubwa ya mwili kufuatia tukio ambalo anadaiwa kumshambulia mtayarishaji wa muziki kwa chupa ya tequila katika kilabu cha Tape, lililopo Mayfair, London.

Chris Brown mwenye umri wa miaka 36 hakuwa mahakamani katika Mahakama ya Southwark Crown siku ya Jumatano wakati wa kusikilizwa kwa dhamana, ambapo jaji aliamuru alipe kiasi cha pauni milioni 5 (takriban shilingi bilioni 16 za Tanzania) kama dhamana kwa mahakama.

Ada ya usalama ni dhamana ya kifedha inayotolewa ili kuhakikisha mshtakiwa anarudi mahakamani. Bw. Brown anaweza kupoteza kiasi hicho cha fedha endapo atakiuka masharti ya dhamana.

Msanii huyo alikuwa akishikiliwa mahabusu tangu alipokamatwa huko Salford siku ya Alhamisi iliyopita, na hapo awali alinyimwa dhamana siku ya Ijumaa.

Hata hivyo, dhamana ilitolewa siku ya Jumatano kwa sharti kwamba alipe pauni milioni 4 mara moja, na pauni milioni 1 nyingine ndani ya siku saba.

Ziara yake ya muziki imepangwa kuanza Amsterdam tarehe 8 Juni, ikiwa na tarehe za maonesho kwenye viwanja na kumbi kubwa katika miji ya Manchester, London, Cardiff, Birmingham, na Glasgow katika mwezi huo wa Juni na Julai.

Mshindi wa tuzo ya Grammy mara mbili, anayejulikana kwa vibao kama Loyal, Run It, na Under the Influence, atarudi mahakamani tarehe 20 Juni, kati ya maonesho yake kwenye Uwanja wa Principality mjini Cardiff na Uwanja wa Tottenham Hotspur jijini London.

Jaji Tony Baumgartner alisema kuwa Chris Brown lazima akabidhi pasipoti yake iwapo hatakuwa safarini kwa ajili ya ziara.

Masharti mengine ya dhamana ni pamoja na:

  • Kuishi kwenye anwani maalum inayojulikana na mahakama,

  • Kutozungumza au kuwasiliana kwa namna yoyote na mlalamikaji,

  • Kutoingia tena katika kilabu cha Tape,

  • Kutoomba nyaraka zozote za usafiri wa kimataifa.

Brown atatakiwa kufika mahakamani mwezi ujao pamoja na mshtakiwa mwenzake, Omololu Akinlolu, mwenye umri wa miaka 38, ambaye anajulikana kwa jina la kisanii HoodyBaby, naye pia anatokea Marekani.

Comments