Mpango maarufu wa Beijing wa Belt and Road utaenezwa hadi katika maeneo ya Afghanistan.
China, Pakistan, na Afghanistan zitaboresha ushirikiano wa pande tatu katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara na usalama, Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatano.
Taarifa hiyo ilichapishwa katika ukurasa wa X (zamani Twitter) baada ya mazungumzo yasiyo rasmi yaliyofanyika Beijing kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Ishaq Dar, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, na Waziri wa Mambo ya Nje wa muda wa Afghanistan Amir Khan Muttaqi.
“Mawaziri hao wa Mambo ya Nje watatu walisisitiza kuwa ushirikiano wa pande tatu ni jukwaa muhimu la kuimarisha usalama wa kikanda na muunganiko wa kiuchumi,” ilisema wizara ya Pakistan.
“Walijadili kuongeza ushirikiano wa kidiplomasia, kuimarisha mawasiliano, na kuchukua hatua za vitendo kuongeza biashara, miundombinu, na maendeleo kama njia kuu za ustawi wa pamoja.”
Islamabad na Beijing pia walikubaliana kupanua mpango wa maendeleo ya miundombinu wa kimataifa wa China, yaani Belt and Road Initiative (BRI), hadi Afghanistan kupitia Mradi wa Uchumi wa China na Pakistan (CPEC).
Mapema mwezi huu, serikali ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban ilitoa taarifa kupitia Wizara yake ya Mambo ya Ndani, ikitoa wito wa “heshima ya pande zote na ushirikiano wa kujenga” na Pakistan pamoja na China.
Kabla ya mkutano wa pande tatu uliofanyika siku ya Jumatano, Waziri Ishaq Dar alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na Wang Yi, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa China alimuelezea Pakistan kama “rafiki wa dhati wa chuma” na “mshirika wa kimkakati wa kila hali ya hewa.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilisema kuwa nchi hizo mbili (Pakistan na China) zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara, uwekezaji, kilimo, na uendelezaji wa viwanda, sambamba na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara.
China ilisema siku ya Jumanne kwamba inaunga mkono Pakistan katika kulinda “uhuru wa kitaifa na mshikamano wa mipaka yake.”
Hatua za Pakistan kuimarisha uhusiano na China na Afghanistan zinakuja kufuatia mzozo mfupi wa kijeshi na India uliomalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano tarehe 10 Mei. Katika mapigano hayo ya siku nne yaliyotokea Mei huko Asia Kusini, Beijing – ambayo kwa muda mrefu imekuwa na uhusiano wa karibu na Islamabad – ilizihimiza pande zote mbili kupunguza mvutano.
Masaa machache kabla ya India na Pakistan kukubaliana kuhusu kusitisha mapigano, Wang Yi alimwapigia simu Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa India, Ajit Doval, na kuonyesha matumaini kuwa New Delhi na Islamabad “wangebaki watulivu na wenye kiasi, wakashughulikia tofauti zao kwa mazungumzo na mashauriano, na kuepuka kuzidisha hali hiyo.”
Siku ya Jumatatu, afisa kutoka taasisi ya tafiti iliyo chini ya Wizara ya Ulinzi ya India aliiambia Bloomberg kuwa China iliiwezesha Pakistan kwa msaada wa ulinzi wa anga na satelaiti wakati wa mzozo huo wa kijeshi wa hivi karibuni katika Asia Kusini.
Comments
Post a Comment