Afrika Kusini Yaomba Wakulima Weupe Wasihamie Marekani

Kundi la Waafrika wenye asili ya Kiholanzi (Afrikaners) limeomba hifadhi ya kisiasa nchini Marekani, likidai kuteswa kwa misingi ya rangi.


Makamu wa Rais Paul Mashatile amewaomba wakulima katika Maonesho ya Kilimo ya NAMPO Harvest Day 2025 wasihame Afrika Kusini kuelekea Marekani
, akiahidi kushughulikia malalamiko yao, ikiwemo suala la usalama na uhalifu.

"Kweli, wakulima tuliokutana nao hapa leo wanasema wanafurahia kubaki Afrika Kusini, na wanachohitaji tu ni sisi kushirikiana nao kutatua changamoto wanazokabiliana nazo," alisema Mashatile.

Aliyasema hayo siku ya Alhamisi wakati akizungumza na vyombo vya habari pembeni ya maonesho ya NAMPO Harvest Day. Tukio hilo linafanyika katika NAMPO Park, mkoani Free State, ambapo lilianza Mei 13 na linatarajiwa kuhitimishwa siku ya Ijumaa.

Mashatile aliwaambia waandishi wa habari kuwa wakulima waliokuwepo kwenye tukio hilo wamesema hawana nia ya kuondoka Afrika Kusini kwenda Marekani.

Pia alikiri kuwa uhalifu bado ni tatizo kubwa linalowakabili wananchi. Mashatile aliwasihi wale wanaofikiria kuhama nchi wabaki Afrika Kusini.

Waafrika Weupe wa Afrika Kusini (White Afrikaners) kwa muda mrefu wamekuwa wakieleza hofu kuhusu usalama wao, na Mashatile alisema kuwa serikali lazima ifanye kazi pamoja na wakulima kushughulikia changamoto zao.

“Moja ya changamoto hizo ni barabara za vijijini. Wanataka tushirikiane nao kulitatua hilo,” alisema.

“Halafu kuna suala la usalama vijijini, kwa sababu tunajua kwa miaka mingi watu wa maeneo ya kilimo wamekuwa wakishambuliwa, uhalifu ni mwingi... Wanataka tushirikiane nao kulitatua hilo ili tuweze kushughulikia matatizo hayo.”

“Wanataka tushirikiane nao kuhakikisha wanapata masoko, yakiwemo masoko ya kimataifa, na pia upatikanaji wa fedha. Hayo ni baadhi ya mambo wanayotueleza: kuwa tukishirikiana nao kwenye mambo haya, hawana tatizo, wao ni wazalendo wa Afrika Kusini, wanataka kubaki hapa, hawana mpango wa kuondoka.”

“Tunawahimiza wale wanaofikiria kuondoka kubaki, hakuna sababu ya kuondoka. Tushirikiane pamoja tujenge nchi hii nzuri kwa pamoja.”

Mapema wiki hii, IOL News iliripoti kuwa Waafrika Weupe 49 (Afrikaners) walipewa hifadhi ya kisiasa (asylum) na waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles karibu na Washington, D.C, siku ya Jumatatu.

Kundi hilo liliondoka Afrika Kusini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo kwa ndege ya kukodishwa ya Omni Air International.

Walidai kuwa walikuwa wakikimbia ubaguzi na vurugu nchini Afrika Kusini, jambo ambalo limesababisha mjadala wa kimataifa huku kukiwa na madai yanayoongezeka — ingawa mengi hayajathibitishwa — kuhusu mateso na mauaji ya wakulima yanayowalenga Waafrika Weupe.

Rais Cyril Ramaphosa amepuuzilia mbali madai kwamba Waafrika Weupe (Afrikaners) wanaohamia Marekani ni wakimbizi halali.

“Tumeeleza wasiwasi wetu kwa sababu watu hao wanaoshawishiwa kwenda Marekani hawafai katika tafsiri ya mkimbizi,” alisema Rais Ramaphosa katika mkutano wa Africa CEO Forum mapema wiki hii.

“Mkimbizi ni mtu anayelazimika kuondoka nchini mwake kwa kuogopa kuteswa kisiasa, kidini, au kiuchumi.”

Alisisitiza kuwa wale wanaoondoka hawateswi.

“Hawafukuzwi, unajua, wala hawatendewi vibaya. Wanaondoka kwa sababu, dhahiri yake, hawataki kukumbatia mabadiliko yanayoendelea nchini mwetu kwa mujibu wa katiba yetu,” alisema.

Wakati huo huo, Rais Ramaphosa anatarajiwa kuzuru Marekani tarehe 21 Mei kwa ajili ya kukutana na Rais Donald Trump katika Ikulu ya White House.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini, ziara hiyo ya kikazi ya siku nne inalenga “kurejesha uhusiano wa kimkakati” kati ya nchi hizo mbili na kupinga mitazamo hasi kuhusu hali ya kijamii na kisiasa ya Afrika Kusini, hasa kuhusu masuala ya rangi.

Trump hapo awali alidai kuwa wakulima weupe wanauawa kikatili na ardhi yao inaporwa nchini Afrika Kusini — kauli zilizozua ukosoaji mkubwa kimataifa na wasiwasi kuhusu upotoshaji wa taarifa.

Wakati wa ziara yake, Ramaphosa anatarajiwa kuthibitisha tena dhamira ya serikali yake ya kujenga demokrasia isiyo na ubaguzi wa rangi na inayojumuisha watu wote, pamoja na kushughulikia mjadala wa kimataifa kuhusu uhamiaji wa Waafrika Weupe na maombi yao ya hifadhi.


Comments